Thursday, July 10, 2014

JAJI MUTUNGI APEWA TAHADHARI NA CHADEMA MTWARA



Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi apewa tahadhali kali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mtwara, kuacha  kukiingilia chama katika katiba yake kwa kutoa taarifa zenye lengo hasi kwa maendeleo na ukuaji wa demokrasia nchini
Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo mkoani mtwara, Kasim Bingwe alisema Jaji Mutungi kukiingilia chama hicho katika shughuli zake za halali ni kinyume na majukumu ya ofisi yake kwa mujibu wa sheria na matarajio ya wananchi katika kujenga demokrasia nchini.
“Msajili anatambua kuwa huu ni ubakaji wa demokrasia na pia anaendelea kutolea hoja mambo yasiyo na mashiko huku akinyamazia mambo yanayolalamikiwa kukwaza demokrasia nchini, licha ya msajili kudai amepokea malalamiko ya wanachama wa CHADEMA wakiwemo waliofukuzwa, iweje ayatoe leo kwenye vyombo vya habari huku akijua kuwa kifungu kinacholalamikiwa kilifutwa na katiba mpya ya 2006?” alihoji.
Mwenyekiti  huyo wa chama cha demokrasia na maendeleo mheshimiwa Bingwe aliongezea kwa kusema:
 “Hivi msajili ameshindwa kuona kuwa wanachama wa chama cha CCM wameanzisha na kuendeleza kampeni za uchaguzi wa 2015 kabla ya wakati huku akijua kuwa hilo ni kinyume cha Katiba na sheria ya uchaguzi?.....inaonekana msajili haoni vijembe vya makundi ndani ya CCM kugombea uongozi kwenye chama chao kabla hata ya muda jambo lililosababisha baadhi yao kuadhibiwa.
Anaongeza kuwa kitendo cha msajili kutamka kuwa mazuio kwa uongozi wa CHADEMA kujihusisha na mambo ya chama kumezua mtafaruku miongoni mwa wanachama na miongoni mwa wapenda chama, hivyo kuwaweka katika hali tete.
“Jambo hili limetusababishia usumbufu wa kujibu mambo yasiyo na tija kwa jamii huku tukiacha kutekeleza majukumu ya ndani ya chama na jamii katika ujenzi wa demokrasia na uchumi wa jamii,” alisema Bingwe.
Hivi karibuni msajili alinukuliwa akizungumza na vyombo vya habari akikaripia na kuwazuia viongozi wakuu wa Chadema kutogombea tena nyadhifa zao, kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja katiba ya chama hicho.

0 comments:

Post a Comment