Monday, April 25, 2016

Barabara ya Mwenge hadi Morocco Iliyojengwa Kwa Fedha za Sherehe za Uhuru Yakamilika kwa asilimia 95


Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa  amekagua  mradi wa upanuzi wa barabara ya Mwenge  hadi Morocco yenye kilomita 4.3 ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 95.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara hiyo  Prof.Mbarawa ameeleza kuwa tayari njia tano zimeanza kutumika kuanzia eneo la Mwenge hadi Kijitonyama zenye urefu wa  kilomita 2 huku kilomita nyingine 2.3 zikiwa katika harakati za mwisho za kukamilishwa.
“Serikali imedhamiria katika kuhakikisha kuwa  inatatua kero ya  msongamano wa magari kwa kufanya upanuzi wa njia  muhimu ili kurahisisha hali ya usafiri jijini Dar es Salaam ” alisema Prof.Mbarawa.
Aliongeza kwa kusema hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alizindua mradi wa daraja la Kigamboni linalounganisha kurasini na Kigamboni pamoja na kuweka  jiwe la msingi  kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa  flyover katika eneo la Tazara.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi  Patrick Mfugale ameeleza kuwa  mradi huo umekabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo uhamishaji wa mabomba ya maji safi na maji taka katika eneo la Makumbusho na Mwenge ili kuendelea na ujenzi.
Novemba 30 mwaka jana  Rais John Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi bilioni nne kilichopangwa kutumika katika shamrashamra za siku ya Uhuru kitumike katika kazi ya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 ili kuiunganisha barabara hiyo na ile ya Mwenge – Tegeta yenye urefu wa KM 12 .

0 comments:

Post a Comment