• This is Slide 1 Title

    This is slide 1 description. Go to Edit HTML and replace these sentences with your own words. This is a Blogger template by Lasantha - PremiumBloggerTemplates.com...

  • This is Slide 2 Title

    This is slide 2 description. Go to Edit HTML and replace these sentences with your own words. This is a Blogger template by Lasantha - PremiumBloggerTemplates.com...

  • This is Slide 3 Title

    This is slide 3 description. Go to Edit HTML and replace these sentences with your own words. This is a Blogger template by Lasantha - PremiumBloggerTemplates.com...

Saturday, April 30, 2016

WAPINZANI WABUNI MBADALA WA KURUSHA YANAYOJIRI BUNGENI

Wabunge wa CCM jana waliibuka kidedea walipowazidi wenzao wa upinzani kwa kura za sauti “Siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni. 

Hiyo ilitokea jana wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utumishi na Utawala Bora) na kuzua mvutano mkali uliosababisha bajeti hiyo ipitishwe kwa utaratibu wa wabunge kutohoji kitu chochote (guillotine).

Wakati hoja yao hiyo ikipingwa kila kona, tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, wabunge hao wa upinzani sasa wamebuni mbinu mpya ya kujirekodi wenyewe wakati wakichangia mijadala mbalimbali bungeni na kurusha sauti zao kwenye mitandao ya kijamii na kupeleka sauti hizo kwenye redio zilizopo katika maeneo ya majimbo yao.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe ndiye aliyeibua hoja hiyo akitaka kushika mshahara wa waziri kwa maelezo kuwa kuzuia Bunge kurushwa ‘live’ ni kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.

Hoja hiyo iliungwa mkono na  Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili (Viti Maalumu -Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa Mbarouk (Tanga Mjini - CUF).

Wabunge wa CCM waliopewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuchangia hoja hiyo ni Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini), Kangi Lugola (Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja na Waziri Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.

Ilivyokuwa  Bungeni

 Baada ya Salehe kutaka ufafanuzi wa kina huku akisisitiza kuwa uamuzi huo unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari, Kairuki alisema kwa mujibu wa Ibara ya 18 na 100 ya Katiba zinazozungumzia uhuru wa kupata habari, uamuzi huo ni sahihi na hakuna mwananchi aliyenyimwa taarifa.

Maelezo hayo yalipingwa na Salehe, safari hii akifafanua kuwa matangazo ya Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani wakiondolewa na kuonyeshwa wa CCM pekee.

Alitaka vyombo vya habari vya elektroniki kuruhusiwa kurekodi shughuli za Bunge na kurusha maudhui wanayoyataka, badala ya kupewa video na studio ya Bunge ambayo huondoa michango na hoja za wapinzani.

Mchungaji Msigwa, Masoud Abdallah, Kamili, Matiko waliungana na Salehe na kusisitiza kuwa nchi nyingi barani Afrika zinarusha ‘live’ matangazo ya Bunge huku wakihoji sababu za TBC kurusha moja kwa moja harusi na kushindwa kuonyesha shughuli za Bunge.

Mbarouk alikwenda mbali akitaka Bunge kuanza shughuli zake usiku ili kuendana na utetezi wa Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuwa usiku wananchi wengi wanakuwa majumbani mwao hivyo wanapata nafasi nzuri ya kufuatilia Bunge.

Matiko: Juzi Rais John Magufuli kazindua Daraja la Kigamboni, TBC ilikata matangazo ya Bunge ili kuonyesha uzinduzi huo. Yaani ya kwenu mnataka yaonyeshwe ila haya ya Bunge yasionekane. Mnakiuka demokrasia.

Ghasia: Demokrasia siyo Bunge kuonyeshwa ‘live’. Wakulima na wafugaji hawawezi kuona Bunge asubuhi ndiyo maana yanarushwa usiku. 

Serukamba: Mbona wabunge wa Chadema wanaonyeshwa katika matangazo ya TBC. Hoja kwamba maagizo ya Serikali hayatawafikia watendaji si kweli.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema wapinzani hawajiamini na hawaaminiki huku akiwataka wasome ibara ya 100 ya Katiba; “Bunge kuonyeshwa au kutoonyeshwa hakuongezi kitu jimboni. Wanaozungumza ni wabunge siyo televisheni.”

Akihitimisha hoja, Kairuki alipinga maelezo ya Salehe na kutoa mfano wa nchi ambazo matangazo ya Bunge hayarushwi moja kwa moja.

Kutokana na mvutano huo Chenge aliwahoji wabunge wanaoafiki hoja ya Salehe waseme “ndiyooo”, wapinzani pekee wakasema ndiyoo, aliposema wasioafiki waseme siyo, wabunge wa CCM kutokana na wingi waliitikia kwa sauti kubwa siyoooo, na Chenge akasema anadhani wasioafiki wameshinda. 

Wapinzani  Waamua Kujirekodi kwa simu

Kwa zaidi ya mara tano,wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakijirekodi ndani ya ukumbi wa Bunge kwa kutumia simu zao za mkononi, wanapotoka nje huulizana kama wameshatumia video na sauti hizo katika mitandao ya kijamii.

Juzi, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara baada ya kumaliza kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utawala Bora) alirusha sauti yake katika mitandao ya kijamii na kusema hiyo ni moja ya njia ya kuwafanya wananchi wajue kinachoendelea bungeni.

465 KUSUBIRI KUNYONGWA

IDADI ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994. 

Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.

Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Wanaharakati 

Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo.

Baadhi ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.

Hata hivyo, Mponezya alisema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.

“Tume inasisitiza Serikali iangalie upya hukumu hii na kuiondoa kwa sababu ya utekelezaji wake. Tangu mwaka 1994 hadi leo watu 465 wanasubiri adhabu hiyo, hakuna aliyenyongwa. Kila mlango unapogongwa unahisi ni wewe kumbe la, tunadhani iondolewe maana haitekelezwi,” alisema Mponezya.

Wananchi wagawanyika 

Tume hiyo ilikiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu hukumu hiyo. 

Wapo wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo, alikiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.

“Tume kadhaa zilizoundwa kupata maoni ya wananchi, zilitoa matokeo kuwa wananchi wengi bado hawataki adhabu iondolewe, wanataka iendelee kuwapo, sasa Serikali inafanya kazi kwa matakwa ya wananchi, si vinginevyo,” alisema Mulumbo.

Akifafanua zaidi, alisema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni mwafaka kufuta adhabu hiyo. 

Marais 

Kuhusu marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.

Alisema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini. 

“Siwasemei kwamba imani zao ni sababu, lakini huenda ni sababu.Ila kisheria rais hahukumiwi akisaini hukumu hiyo, sasa hilo mimi siwezi kulisemea ila sheria zinaweza kuangaliwa zaidi, ili zimpe rais nafasi ya kumpa mhusika kifungo cha maisha. 

“Lakini hapo napo kuna mtazamo mwingine, maana kuna hoja kwamba kwa nini aliyeua na kupatikana na hatia afungwe maisha. Je, iko wapi haki ya aliyeuawa?” Alifafanua Mulumbo kwa mtazamo wake.

Wanaoipenda 

Mwanasheria wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro, ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alisema  kwamba, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo, umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.

Senkoro alisema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.

“Wengi wa jamii yetu wanataka hukumu iendelee kuwapo mpaka hapo mauaji kwa albino yatakapokoma na itekelezwe. Wauaji wa albino wanaua kwa imani si tabia, wanatumwa na watu wenye fedha, kiungo kinauzwa Dola za Marekani 2,000, tena tunaona wanaokamatwa ni vidagaa, bado mapapa hatuyaoni, tunaomba Serikali (ya Magufuli) iwatafute vigogo na tuone hukumu hii ikitekelezwa ili kumaliza imani hizi zinazowanyima haki baadhi yetu ya kuishi,” alisema Senkoro.

Pamoja na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu, bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta adhabu ya kifo.

Mkutano huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia 50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa zinatajwa kuwa kubwa. 

Nchi zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa.

Dr.MPANGO: Serikali ya JK haikukomba fedha Hazina

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amesema Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete haikukomba fedha katika Hazina kama ambavyo baadhi ya wabunge wamedai, hata Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), lilifanya tathmini na kutoa taarifa safi.

Dk Mpango alieleza hayo bungeni jana mjini hapa, wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia mjadala wa wizara mbili zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Utawala Bora, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walisema Serikali ya Awamu ya Nne, ilikomba fedha zote Hazina na kusababisha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, kukuta Hazina haina fedha.

Akijibu hoja hiyo, alisema hakuna ushahidi ulioitia hatiani Serikali ya Awamu wa Nne kuhusu kukomba fedha Hazina na kwamba IMF na wadau wengine wa kimataifa, walifanya tathmini huru ya bajeti na mwenendo wa uchumi nchini na taarifa yao ya mwisho waliitoa Desemba mwaka 2015.

Katika ripoti hiyo hakuna mahali ilipoonesha nchi ilikuwa na hali mbaya ya fedha na kwamba kwa kudhihirisha hilo, vigezo vya kimataifa vilionesha bayana kuwa Deni la Taifa ni himilivu na nchi bado inakopesheka na imeendelea kulipa mishahara watumishi wake pamoja na madeni mengine bila kutetereka.

Alisema Serikali iliendelea kulipa madeni mengi na hakuna kilicholegalega, huku ikiendelea pia kugharimia shughuli za mihimili yote, ikiwemo Bunge, usalama wa nchi na kuendelea kulipa madai ya makandarasi na watoa huduma wengine.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imerithi mambo mengi mazuri yaliyofanywa na serikali za awamu zilizopita, ikiwemo uchumi imara, umeme uliosambazwa maeneo mengi vijijini na miundombinu.

8,236 HEWA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki

SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kutaja idadi ya watumishi hewa kuwa ni 7,200, msako unaoendelea katika utumishi wa umma, umetoa takwimu mpya ambapo sasa watumishi hao wamefikia 8,236.

Katika hatua nyingine, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ambao wamefunguliwa kesi mahakamani kutokana na ubadhirifu, ambao wamekuwa wanatumia magari na mafuta ya umma na kujilipa posho wanapokwenda kwenye kesi zao, wataanza kuchukuliwa hatua kali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema hayo bungeni jana wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.

Akizungumzia wafanyakazi hewa, Waziri Kairuki alisema kati ya Machi Mosi na Aprili 24, mwaka huu, Serikali imebaini kuwepo kwa watumishi hewa 8,236, idadi inayoonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa baada ya hivi karibuni Rais kuripoti kuwepo wafanyakazi hewa 7,200.

Alisema katika idadi hiyo, wafanyakazi hewa 1,614 wameripotiwa kutoka Serikali Kuu huku wengine 6,622 wakiripotiwa kutoka Serikali za Mitaa, na kufanya ongezeko lao kufikia 2,737.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, kuwepo kwa wafanyakazi hao hewa katika utumishi wa umma kumeisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 15.4, ambazo zingeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika kushughulikia hilo, Serikali imelazimika kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 56 ambao walibainika kuhusika kufanikisha malipo ya mishahara kwa watumishi hao hewa na hatua mbalimbali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

‘’Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao na endapo watabainika kuwa na makosa kisheria, watalazimika kurejesha fedha za Serikali zilizopotea kutokana na malipo hayo hewa ya mishahara,” alisema Kairuki.

Kuhusu wakurugenzi wa halmashauri wenye kesi za ubadhirifu mahakamani, Waziri Kairuki alisema Serikali inafanya uchunguzi kuhusu wakurugenzi hao ambao kutokana na kuwa na kesi mahakamani, wanatumia fedha na rasilimali za Serikali kwenda kuhudhuria kesi zao.

“Zipo taarifa hizo kwamba wakurugenzi hawa wanakwenda katika kesi hizo wakiwa wamejilipa posho za kujikimu za Serikali wao na madereva wao lakini pia wakitumia magari na mafuta ya Serikali. Ikibainika kuwa wapo wakurugenzi kama hawa hatua kali zitachukuliwa kwao mara moja,” alisema Waziri Kairuki.