Idhaa ya utangazaji ya BBC leo
imezindua mradi wa kitaifa unaohusisha wanafunzi katika utangazaji wa habari.
Wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali
ya dunia wamepata fursa ya kuandaa ripoti kuhusu maswala mbalilmbali
yanayowahusu. Kutoka mji mkuu wa Kenya Nairobi
tunakuletea ripoti iliyoandaliwa na wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya
Starehe ambapo hawaruhusiwi kubeba simu za mkononi shuleni.
Karibu katika shule ya Starehe boys
centre mjini Nairobi. Shule yetu inajulikana kwa umahiri katika masomo hasa
katika mitihani ya kitaifa.
Ili kuimarisha umakinifu wetu
masomoni, haturuhisiwi kubeba simu shuleni.
Tuna vyumba vya computa vyenye
internet lakini tunavitumia tu kwa masomo na utafiti peke yake.
Haturuhusiwi kutumia computa kwa
mawasiliano kupitia barua pepe au mitandao ya kijamii kama vile Facebook na
Twitter.
Lakini hilo halituzuii kuwasiliana
na marafiki zetu hasa wasichana katika shule zingine.
Matumizi
ya simu yamepelekea watu wengi kusahau uandishi wa barua
Inatubidi kutumia njia ya
zamani,tunaandika barua,lakini sio barua za kawaida.
Ni barua zilizoandikwa kwa umakinifu
na kurembeshwa kwa kalamu zenye rangi aina mbalimbali na hua tunaziandika
wakati wa mapumziko.
Katika maktaba ya shule nakutana na
baadhi ya marafiki zangu wakiandika barua baada ya masomo.
''Mara nyingi tunaandika barua hizi
kwa marafiki zetu wasichana kwa hivyo tunaziandika kwa njia spesheli ili
kupasha hisia zetu sawasawa'', anasema Charles huku akitabasamu.
Baadhi ya wanafunzi wanaamini
kuandika barua ni njia bora kwani inawapa fursa kutumia vipaji vya usanii.''
Napenda sana sanaa ya uchoraji na
pia matumizi ya lugha hasa ya mapenzi '', anasema Moses huku akirembesha
bahasha kwa kutumia kalamu zenye rangi tofauti.
Kwa mpenzi wangu ....
''Namwandikia rafiki yangu wa karibu
sana nilimuona mara ya mwisho wakati wa likizo na nahisi nimemkosa sana'',
anaongeza.
Baada ya kuandika barua hizo,
tarishi anatumia pikipiki yake kuzisafirisha hadi katika shule ya wasichana ya
Loreto Msongari, upande mwingine wa mji.
Wasichana wanafurahia kuzipokea na
baadhi yao wananieleza fikra zao kuhusu matumizi ya barua kama njia ya
kuwasiliana.
''Nimependezwa sana na barua
niliyopokea ,imerembeshwa kwa rangi aina mbalimbali'' anasema Stacy.
'' Nafikiri ni bora kutumia barua
kuwasiliana kwasababu njia zingine kama simu zinaweza kutufanya tusizingatie
masomo'', anaongeza.
Wasichana kutoka shule jirani
wakisoma barua kutoka kwa wapenzi wao katika shule ya Starehe
Naye Stephanie aliniarifu kuwa
alifurahishwa sana na barua aliyopokea, '' alinifurahisha sana naona alitumia
lugha safi sana, naona tuendelee matumizi ya barua'', anasema.
Nilimtaka msichana Angel kunieleza
kilichomvutia zaidi katika barua aliyopokea.
'' Nilifurahia pale aliponiambia
kuwa nywele zangu ndefu zinapendeza na kwamba nina tabasamu ya kuvutia kiasi
kwamba inaweza kumfanya awe kipofu'' anasema huku akicheka.
Huku vijana wengine duniani wakiwasiliana na
marafiki zao kwa kutumia simu za mkononi imebidi sisi kutumia mbinu ya kuandika
barua kufanya hivyo na inatufaa na kutufurahisha
Habari kutoka BBC