Loliondo. Polisi wawili, PC Isaack na PC Mabrouk wamejeruhiwa
baada ya kupigwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni Wamasai (morani) katika
Kijiji cha Ololosokwani, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.
Tukio hilo pia limesababisha watu 25 kutiwa
nguvuni, akiwamo mbunge wa zamani wa Jimbo la Ngorongoro, Merthew ole
Timan na madiwani wawili.
Inadaiwa tukio hilo limetokana na kuchochewa na
uhasama kati ya wananchi na polisi kutokana na migogoro ya ardhi katika
wilaya hiyo, limesababisha PC Isaack kuvunjwa mkono na jana alihamishiwa
Hospitali ya Seliani Arusha Medical Center kwa matibabu zaidi baada ya
hali yake kuwa mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashimu Mgandilwa
alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi
kukamilika.
“Ni kweli polisi wawili wamepigwa na jeshi
liliendesha msako wa kuwatafuta watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata watu
25 kwa tuhuma za kushambulia polisi, uchochezi, kufanya mikusanyiko
isiyo halali na kupanga mbinu za uhalifu,” alisema Mgandilwa.
Alisema chanzo cha kupigwa polisi ni operesheni ya
kuchunguza wahamiaji haramu ambayo inapingwa na wananchi na viongozi wa
eneo hilo.
Hata hivyo, viongozi waliokamatwa kuhusu tukio hilo, jana walipata dhamana.
Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Iyanick Ndoinyo na
Diwani wa Oldonyosambu Daniel Ngoitiko, walisema wanapinga tukio la
kupigwa polisi hao, lakini chanzo ni polisi kukamata pikipiki za
wananchi na kudai faini kubwa.
Iyanick alisema ingawa ni kweli kuna uhasama wa
polisi na wananchi, lakini taarifa alizopata ni kwamba polisi wadai
faini kubwa na kisha kumpiga kijana mmoja wa Kimasai.
“Sisi kama viongozi tunapinga kupigwa polisi, pia kukamatwa kwetu ni kudhalilishwa,” alisema.
Alisema, “Hatupingi hatua ya Serikali kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.”
Naye Ngoitiko alisema wao kama viongozi wanalaani
tukio hilo na wanataka Serikali kufanya uchunguzi kujua chanzo badala ya
kukamata watu bila kuwa na ushahidi.
Chanzo