SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) limeelezea kuridhishwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutekeleza mapendekezo yake, ikiwemo kuundwa kwa chombo cha majadiliano kitaifa chenye lengo la kuleta ufanisi sehemu za kazi na kuondoa migogoro.
Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi alisema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mafanikio na changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sekta binafsi.
Mwinyi alisema kitendo cha Serikali ya Mapinduzi kukubali kuundwa kwa chombo hicho na kuanza kutekeleza majukumu yake kwa kiasi kikubwa kitasaidia kuleta ufanisi sehemu za kazi na kuondoa malumbano ambayo yamekuwa yakijitokeza baina ya Serikali na Shirikisho hilo kuhusu maslahi na stahili za wafanyakazi nchini.
“Tunaipongeza Serikali hii kukubali kuunda chombo cha majadiliano kitaifa ambacho kimekuwa kilio chetu kwa muda mrefu,” alisema.
Akifafanua, Mwinyi alisema chombo cha majadiliano na Serikali kinaundwa na wajumbe 10 kutoka Serikalini na vyama vya wafanyakazi na Mwenyekiti wake ni Naibu Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi pamoja na wajumbe wengine kutoka katika ZATUC.
Alisema tayari vikao mbalimbali vimefanyika kwa mujibu wa kalenda ambavyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuzipitia changamoto mbalimbali zilizopo na kupatiwa ufumbuzi.
Aidha Mwinyi alisema tayari Mahakama ya Kazi imeanza kusikiliza kesi mbalimbali zinazohusu wafanyakazi wa sekta mbalimbali na kutolewa hukumu, hatua ambayo imesaidia kuondoa mlundikano wa mashauri ya malalamiko.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi kwa sababu itasaidia kutoa haki kwa wafanyakazi kuweza kusikilizwa mashauri yao mbele ya mahakama na hivyo kuimarisha ufanisi na uzalishaji sehemu za kazi.
Hata hivyo, Mwinyi alisema wafanyakazi wa Zanzibar ikiwemo wa sekta binafsi na serikali wanakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi haraka.
Alitaja moja ya changamoto hizo ombi la kutaka kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa Serikali kupanda zaidi kutoka cha sasa cha Sh 150,000 na sekta binafsi Sh 145,000.
Alisema viwango hivyo vimepitwa sana wakati. Alisema mwaka 2000 shirikisho hilo lilitafuta mshauri mwelekezi kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu kiwango cha mishahara ambapo utafiti huo ulikamilika mwaka 2011 na kuonesha kwamba kiwango cha chini kwa wafanyakazi wa serikali kilipaswa kuwa Sh 350,000.
Alitaja changamoto nyingine zinazowakabili wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa ni tofauti ya mishahara kutoka kwa wenzao walio katika serikali ya Muungano, tofauti ambayo ni kubwa wakati wote ingawa wanatumia soko moja la bidhaa.