Thursday, April 28, 2016

NAIBU SPIKA: BWEGE BUNGENI


Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.

Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.
Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”
Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.
Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.
“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.
Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika.
“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,”alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati.
Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba? 
Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?
Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.
Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.
Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu.

Related Posts:

  • KIZIMBANI KWA KUHIFADHI WAHAMIAJI HARAMU Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga. MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kagoli amefikishwa mahakamani kwa kosa la kuhifadhi wahamiaji haramu nyumbani kwake na kuwatumikisha mashambani. Kagoli ambay… Read More
  • NAPE KUDILI NA MAJIPU KWENYE SANAA Waziri wa Habari,Utamaduni,sanaa na michezo nchini,Nape Nnauye ametaja mambo manne ambayo ni vikwazo ndani ya sekta ya sanaa ya filamu nchini na kuyaita kwamba ni majipu huku akisisistiza kwamba serikali itakwenda kutunga s… Read More
  • Serikali ya China kudhibiti dini Chama cha kikoministi cha China kimepewa mamlaka ya kudhibiti dini nchini humo. Kiongozi wa Uchina, Xi Jinping, amesema makundi ya kidini lazima yakubali kudhibitiwa na chama cha kikoministi. Akizungumza katika mkutano wa s… Read More
  • Serikali ya China kudhibiti dini Chama cha kikoministi cha China kimepewa mamlaka ya kudhibiti dini nchini humo. Kiongozi wa Uchina, Xi Jinping, amesema makundi ya kidini lazima yakubali kudhibitiwa na chama cha kikoministi. Akizungumza katika mkutano wa s… Read More
  • Mkataba wa LugumiHii hapa ni taarifa ya Utekelezaji Ya Kamati Ndogo ya PAC Kuhusu Mkataba wa Lugumi … Read More

0 comments:

Post a Comment