Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira ilisema wafungwa 580 wataachiwa huru, huku wengine 2,971 watapunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao.
Alisema rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliwataja watakaonufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wenye ugonjwa wa ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wapo kwenye hatua za mwisho. Wengine ni wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, wajawazito na wale waliongia na watoto gerezani.
Wafungwa wengine watakaonufaika na msamaha huo ni wenye ulemavu wa akili ambao wamethibishwa na jopo la waganga kuwa wana tatizo hilo.
Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema msamaha huo hautawagusa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kifungo cha maisha jela.
Pia, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, upokeaji na utoaji rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, unyang’anyi kwa kutumia silaha na kubaka ni miongoni mwa waliokosa msamaha huo.
Wengine ambao hawataguswa na msamaha huo ni wale wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, wizi wa magari na pikipiki, kuwapa mimba wanafunzi na ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Wafungwa wengine watakaoendelea kubaki magerezani ni wale waliohukumiwa kutokana na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, utekaji wa watoto, biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya binadamu na waliojaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
Katika maadhimisho ya Uhuru yaliyofanyika Desemba 9, 2015, Rais Magufuli aliwasamehe wafungwa 2,336, kati ya hao 117 waliachiwa huru huku 2,219 wakipunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao.
Kwa idadi hiyo mpaka sasa wafungwa 5,887 wamenufaika na msamaha wa Rais Magufuli tangu aingie madarakani baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015.
0 comments:
Post a Comment