Sunday, May 10, 2015

POLISI HOI KWA KIPIGO, MBUNGE AKAMATWA

Loliondo. Polisi wawili, PC Isaack na PC Mabrouk wamejeruhiwa baada ya kupigwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni Wamasai (morani) katika Kijiji cha Ololosokwani, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.
Tukio hilo pia limesababisha watu 25 kutiwa nguvuni, akiwamo mbunge wa zamani wa Jimbo la Ngorongoro, Merthew ole Timan na madiwani wawili.
Inadaiwa tukio hilo limetokana na kuchochewa na uhasama kati ya wananchi na polisi kutokana na migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo, limesababisha PC Isaack kuvunjwa mkono na jana alihamishiwa Hospitali ya Seliani Arusha Medical Center kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashimu Mgandilwa alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
“Ni kweli polisi wawili wamepigwa na jeshi liliendesha msako wa kuwatafuta watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata watu 25 kwa tuhuma za kushambulia polisi, uchochezi, kufanya mikusanyiko isiyo halali na kupanga mbinu za uhalifu,” alisema Mgandilwa.
Alisema chanzo cha kupigwa polisi ni operesheni ya kuchunguza wahamiaji haramu ambayo inapingwa na wananchi na viongozi wa eneo hilo.
Hata hivyo, viongozi waliokamatwa kuhusu tukio hilo, jana walipata dhamana.
Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Iyanick Ndoinyo na Diwani wa Oldonyosambu Daniel Ngoitiko, walisema wanapinga tukio la kupigwa polisi hao, lakini chanzo ni polisi kukamata pikipiki za wananchi na kudai faini kubwa.
Iyanick alisema ingawa ni kweli kuna uhasama wa polisi na wananchi, lakini taarifa alizopata ni kwamba polisi wadai faini kubwa na kisha kumpiga kijana mmoja wa Kimasai.
“Sisi kama viongozi tunapinga kupigwa polisi, pia kukamatwa kwetu ni kudhalilishwa,” alisema.
Alisema, “Hatupingi hatua ya Serikali kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.”
Naye Ngoitiko alisema wao kama viongozi wanalaani tukio hilo na wanataka Serikali kufanya uchunguzi kujua chanzo badala ya kukamata watu bila kuwa na ushahidi.

Chanzo

0 comments:

Post a Comment