AFISA uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara Bw. Julius Bujabhi Makwasa amehukumiwa kifungo cha Miaka 7 jela baada ya kupatikana na hatia ya Makosa 34 yakiwepo ya Rushwa.
Mnamo mwaka 2013 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mara ilimfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti Afisa uchaguzi wa Halmashauri hiyo Bwana Julius Bujabhi Makwasa na wenzake wawili wakishitakiwa kwa makosa thelathini na manne yakiwemo ya matumizi mabaya ya fedha za umma, kuisababishia hasara Halmashauri ya Serengeti, kusaidia kutenda kosa, kughushi na kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao.
Washitakiwa wengine katika shauri hilo la uhujumu Uchumi E.C.C 130/2013 lililokuwa likisikilizwa na Hakimu wa Mahakama hiyo Mheshimiwa Ismail Emanuel Ngaile, walikuwa Bi Scola Daudi Mosi ambaye ni mtunza kumbukumbu wa Halmashauri hiyo na Bwana Dickson Julius Makwasa ambaye ni mtoto wa mshitakiwa wa kwanza.
Ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Wakili Martin Makani mbele ya mheshimiwa Ngaile kwamba mshitakiwa wa kwanza Julius Makwasa ambaye majukumu yake yalikuwa pamoja na kuviteketeza vifaa vya uchaguzi muda wa uchaguzi unapopita na mshitakiwa wa pili Scola Mossy ambaye majukumu yake ni pamoja kusimamia kumbukumbu zinazoingia na zinazotoka nje ya Halmashauri hiyo, kwa nafasi zao hizo, walikuwa na jukumu la kuharibu nyaraka za uchaguzi mkuu wa Octoba 2010 kama ilivyokuwa imeelekezwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi.
Katika kutekeleza jukumu hilo ilielezwa kwamba, waliandaa majina ya vibarua na kuingiza majina hewa ishirini na tano (25) kuonyesha kwamba majina hayo hewa pia yalishiriki kuchimba mashimo, kusomba nyaraka hizo za uchaguzi na kuzipeleka kwenye mashimo kisha kuziteketeza kwa moto hivyo kustahili malipo.
Katika udanganyifu huo ilielezwa kwamba, mshitakiwa wa kwanza na wa pili waliweza kuandaa nyaraka za kuipotosha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuwawezesha kujipatia jumla ya shilingi million tatu laki nane na elfu hamsini (Tsh 3,850,000/=) kwa kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri .
Aidha katika mashitaka hayo, mshitakiwa wa tatu Dickson Makwasa ambaye ni mtoto wa mshitakiwa wa kwanza yeye alishitakiwa kwa kosa moja la kusaidia kutenda kosa kwa maelekezo ya baba yake Julius Bujabhi Makwasa, ambapo ilielezwa na upande wa mashitaka kuwa alielekezwa na baba yake kutafuta na alitafuta wanafunzi wenzake na kuwapeleka ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa mtunza fedha na huko walitakiwa kutia sahihi mbele ya majina hewa yaliyokuwa yameorodheshwa kisha kulipwa fedha zilizoainishwa kwa kila jina kama kwamba ni wao walifanya kazi ya kuteketeza vifaa hivyo vya uchaguzi.
Hata hivyo baada ya kupokea fedha hizo wanafunzi hao walitakiwa wazikabidhi kwa mshitakiwa wa tatu na wakazikabidhi, ambaye naye alimkabidhi mshitakiwa wa kwanza ambaye ni baba yake.
Baada ya mahakama kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka na ule wa utetezi iliridhika kwamba mshitakiwa wa kwanza alitenda makosa yote (33) aliyoshitakiwa nayo na hivyo kuhukumiwa kifungo, kulipa faini ya shillingi millioni tano (Tsh.5,000,000/=) au kifungo jela miaka saba na kurejesha fedha jumla ya shilingi million tatu, laki nane na hamsini elfu ( 3,850,000/=) hasara aliyoisababishia Serikali, alishindwa kulipa fedha hizo na kupelekwa jela kuanza kutumikia kifungo.
Mshitakiwa wa pili alionekana hana hatia hivyo mahakama ilimuachia huru, kwa upande wa mshitakiwa wa tatu ambaye kosa lake lilikuwa kusaidia kutenda kosa kwa maelekezo ya baba yake alipatikana na hatia ya kosa hilo na alihukumiwa kulipa faini ya shilingi million moja (TSH.1000,000/=) au kwenda jela miaka mitatu, aliweza kulipa fedha hizo na akaepuka kifungo.
TAKUKURU Mkoa wa Mara inatoa mwito kwa wazazi hasa walio kwenye utumishi wa umma kuacha tabia ya kuwashirikisha watoto katika kufanikisha vitendo vya uvunjaji wa sheria, kwa kuwa kuendelea kufanya hivyo kutapelekea kujenga jamii ya kihalifu kutokana na vijana kuiga tabia za kihalifu zinazoonyeshwa kwao na wazazi.
IMETOLEWA NA
HOLLE J. MAKUNGU
MKUU WA TAKUKURU(M)MARA
MKUU WA TAKUKURU(M)MARA
25 APRILL 2016.
0 comments:
Post a Comment