MBUNGE
wa Nkasi Kaskazini, mkoani Rukwa, Bw. Ally Mohamed Kessy (CCM),
ameitaka Serikali itoe tamko la haraka kuhusu hali ya upatikanaji huduma
za afya katika hospitali za umma.
Alisema hivi sasa maafa
yanayowapata Watanzania kutokana na uhaba wa dawa katika hospitali na
vituo vya afya vilivyopo chini ya Serikali ni zaidi ya vifo
vilivyotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea nchini Rwanda
na Burundi.
Bw. Kessy aliyasema
hayo bungeni mjini Dodoma jana baadaya kuomba mwongozo na kusisitiza
kuwa, hali ya upatikanaji dawa katika hospitali na vituo vya afya ni
mbaya.
“Madhara yanayotokana
na ukosefu wa dawa ni zaidi ya vita vilivyotokea Rwanda na Burundi...
naiomba Serikali iache mzaha na suala hili, itoe tamko haraka ili
Watanzania wajue la kufanya,” alisema Bw. Kessy.
Siku chache zilizopita,
Mbunge wa Kisesa, mkoani Simiyu, Bw. Luhaga Mpina, alilitaka Bunge
kusitisha vikao vyake ili fedha zinazotumika kuwalipa posho, zitumike
kulipa deni ambalo Serikali inadaiwa na Bohari ya Dawa (MSD).
Deni hilo ni sh. bilioni 102 hali inayosababisha MSD ishindwe kumudu gharama za kuagiza dawa nje ya nchi.
Akisisitiza msingi wa
hoja yake, Bw. Kessy alisema kutokana na tatizo hilo, Watanzania wengi
wanapoteza maisha hasa watoto na wajawazito; hivyo ni vyema Serikali
ikatoa tamko la kupatikana ufumbuzi wa tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
Mbunge wa Viti Maalumu,
Esther Bulaya, alisema mashine ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya
kizazi katika Hospitali ya Ocean Road, ni mbovu isipokuwa moja ambayo
nayo inafanya kazi kwa kusuasua hali ambayo inasababisha mateso makubwa
kwa wagonjwa wanawake.
“Hadi sasa, hali ya
huduma za afya pale Ocean Road ni tete, mashine ya uchunguzi wa saratani
ya shingo ya kizazi imekufa, inayofanya kazi ni moja tena kwa
kusuasua...Serikali itoe tamko ili kunusuru maisha ya wanawake, hali ni
mbaya,” alisema.
Akitoa ufafanuzi wa
suala hilo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandyosa, alisema suala la tiba ni muhimu kwa
uhai wa binadamu ambapo Serikali inatambua tatizo lililopo.
Alisema Serikali itatoa
tamko rasmi bungeni hivyo aliwaomba wabunge kuwa na subira ambapo Prof.
Mwandosya, pia alitolea ufafanuzi kuhusu mwongozi ulioombwa na Mbunge
wa Mbozi Magharibi, mkoani Mbeya, Bw. David Silinde (CHADEMA).
Katika mwongozo huo,
Bw. Silinde alitaka Serikali itoe tamko kuhusu madeni ya wakulima wa
mahindi waliyouza kwa Wakala wa Hifadhi ya Taifa (NFRA), yaliyodumu kwa
miezi mitatu lakini Serikali imekaa kimya bila kutoa kauli yoyote.
Bw. Silinde alisema
wakulima hao wamelima mahindi na sasa hawanufaiki nayo kwani mbali na
kuendelea kuidai Serikali, mengine yanaoza kwa kukosa soko na
kuwasasabishia umaskini.
Akijibu hoja hiyo,
Prof. Mwandosya alisema ni kweli suala la wakulima wa mahindi
limezungumza sana ambapo Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, itatoa
tamko la Serikali wiki hii.
Bunge hilo liliendelea
kujadili mpango wa maendeleo ambapo Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph
Mbilinyi (CHADEMA), alidai kusikitishwa na kauli aliyoiita nyepesi.
Kauli hiyo ilitolewa
bungeni na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw.
Bernard Membe kuhusu kuenea kwa habari za Rais wa China kuondoka na meno
ya tembo alipokuja nchini.
Alisema Bw. Membe
alitoa kauli nyepesi ambayo kila akiitafakari anashindwa kuelewa hasa
ukizingatia suala hilo ni nyeti na linagusa masilahi ya Taifa; hivyo
alistahili kulieza Bunge kwa umakini si kama alivyofanya.
“Nimesikitishwa na
kauli ya Waziri Membe, nilitegemea kuona akiliambia Bunge hatua
zilizochukuliwa na Serikali au kuunda tume ili iweze kubaini ukweli wa
jambo hilo badala ya kutoa taarifa za kukanusha bungeni.
“Mbali ya Rais wa China
kuchafuliwa, Taifa letu pia limechafuka kwa sababu suala hili
limezungumzwa katika vyombo vya habari ambavyo vingi ni vya kimataifa,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment