Friday, April 22, 2016

BOMBA LA MAFUTA KUPATA UAMUZI MWISHONI MWA WIKI

Viongozi wa Kenya, Uganda na Tanzania mwishoni mwa wiki wanatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda na Kenya hadi pwani.

Mwaka jana, Kenya na Uganda zilikuwa zinashauriana kuhusu mpango wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, magharibi mwa Uganda, hadi bandari ya Lamu katika Pwani ya Kenya.

Bomba hilo la mafuta lilikusudiwa kutumiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka eneo la Ziwa Albert nchini Uganda na kutoka eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.

Rais Uhuru Kenyatta na Rais Yoweri Museveni walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo ulifaa kuharakishwa.

Lakini Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikutana na Rais Museveni Machi mwaka huu na wawili hao wakakubaliana kuhusu mpango wa kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga katika pwani ya Tanzania.

Baadaye, Rais Magufuli alikutana na makamu wa rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw Javier Rielo na wakaafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo linalokadiriwa kuwa la urefu wa kilomita 1,410 uanze haraka iwezekanavyo.

Kampuni ya mafuta ya Total ndiyo inayofadhili ujenzi huo.

Bw Javier alisema kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa.

0 comments:

Post a Comment