Sunday, April 24, 2016

Wakenya kinara katika London Marathon

Mwanariadha mkenya Eliud Kipchoge nusura avunje rekodi ya duniaya mbio za Marathon alipoandikisha muda wa kasi zaidi katika mbio za London Marathon.

Kipchoge wa Kenya,alihifadhi taji aliloshindwa mwaka uliopita alipoandikisha muda wa kasi zaidi wa saa mbili dakika tatu na sekunde 5 sekunde 8 tu nje ya rekodi ya dunia ya mbio hizo.

Rekodi hiyo ya dunia iliwekwa na mkenya mwenza Dennis Kimetto katika mashindano ya Berlin Marathon mwezi Septemba mwaka wa 2014.

Kipchoge ambaye alikuwa ameandamana na mkenya mwenza Stanley Biwott hadi iliposalia takriban kilomita tatu kufikia kwenye utepe , alipotifua kivumbi na kubaini udedea wake katika mbio hizo za masafa marefu.

Biwott alijifurukuta na kumaliza katika nafasi ya pili huku mpinzani wake katika mbio za mita 5000 Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia akifunga orodha ya tatu bora.

Kufuatia ushindi huo Kipchoge ndiye mwanariadha wa kwanza tangu Martin Lel vilevile wa Kenya aliposhinda taji lake la pili mwaka wa 2008.

Katika kitengo cha wanawake cha mbio hizo ,Mkenya mwengine, Jemima Sumgong, aliyeanguka katika sehemu ya mwanzo mwanzo wa mashindano ya leo alijitahidi na kuibuka mshindi wa mbio za wanawake.

Sumgong, 31, aligonga kichwa chake chini baada ya kutegwa na mwanariadha mpinzani kutoka Ethiopia Aselefech Mergia.

Hata hivyo alijifurukuta kutoika nyuma na kuandikisha muda wa saa mbili dakika 22 na sekunde 58 alipokata utepe na kutawazwa bingwa mwaka huu wa mbio za London Marathon.

Tigist Tufa wa Ethiopia, aliyeshinda mwaka jana, safari hii amekuwa wa pili.

Mkenya mwengine Florence Kiplagat alimaliza katika nafasi ya tatu akitumia muda wa saa mbili dakika 23 na sekunde 39

0 comments:

Post a Comment