Wednesday, October 22, 2014

MADEREVA, MAKONDAKTA UDA KUKIONA



ABIRIA wa mabasi jijini Dar es Salaam, wameshauriwa kusaidia kudhibiti uendeshaji holela na tabia zisizokubalika zinazofanywa na baadhi ya madereva na makondakta kwa kupiga simu zilizochapishwa katika mabasi yote ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Taarifa ya UDA iliyotolewa jijini Da es Salaam jana na Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, George Maziku, ilieleza kuwa utumiaji wa namba hizo utaisaidia pia kampuni kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake.
“Tunawakumbusha wateja wetu pamoja na watumiaji wengine wa barabara kuripoti uzembe wowote au utovu wa nidhamu utakaofanywa na madereva na makondakta wa UDA, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
“Mbali na kuboresha utoaji wa huduma zetu, UDA inalenga kuwa mfano wa kuigwa kwa mabasi mengine ya abiria nchini katika uzingatiaji wa sheria, utoaji wa huduma nzuri kwa wateja na kuwa kichocheo cha kupunguza foleni katikati ya jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Maziku alisema uongozi wa UDA utachukulia kwa uzito mkubwa na kuyafanyia kazi maoni yote yakayokuwa yakitolewa kupitia namba hizo, ili kuondokana na dhana potofu kwamba wamiliki na waendeshaji wa kampuni za magari ya abiria ni watu ambao hawajaelimika.
Alisema  mbali na uwepo wa namba hizo za simu, UDA itaendelea na utekelezaji wa utaratibu wake wa kutuma waratibu kupanda mabasi ya kampuni hiyo na kuripoti juu ya utendaji kazi wa madereva na makondakta wa mabasi hayo.


0 comments:

Post a Comment